Tarehe 4 Machi, 2021
Ni fahari yetu kukutangazia kwamba njia salama na ya faragha ya kupiga simu za sauti na video kati ya mtu na mwingine sasa inapatikana kwenye programu ya WhatsApp kwenye kompyuta.
Katika mwaka uliopita, tumeshuhudia ongezeko la watu wanaopigiana simu kwenye WhatsApp, aghalabu kwa mazungumzo ya muda mrefu. Katika Mkesha wa Mwaka Mpya mwaka jana, tulivunja rekodi kwa kuwa na simu bilioni 1.4 za sauti na video zilizopigwa katika siku moja pekee. Huku kukiwa na idadi kubwa ya watu ambao bado wapo mbali na wapendwa wao na kuendelea kuzoelea njia mpya za kufanya kazi, tunataka mazungumzo kwenye WhatsApp yahisi kana kwamba ni ya ana kwa ana kadiri iwezekanavyo, bila kujali mahali ulipo ulimwenguni au ni teknolojia gani unatumia.
Kupokea simu katika skrini kubwa kunarahisisha kufanya kazi na wafanyakazi wenzako, kuwaona wanafamilia kwa ubora zaidi kwenye kiwambo kikubwa, au kukuruhusu kutumia mikono yako kufanya vitu vingine wakati unazungumza. Ili kufanya upigaji simu kwenye kompyuta uwe na manufaa zaidi, tumehakikisha kwamba inafanya kazi vizuri katika mkao wima au mlazo, inaonekana kwenye kidirisha huru kinachoweza kubadili ukubwa wake kwenye skrini ya kompyuta yako, na ambacho kitakuwa katika sehemu ya juu ya skrini kila wakati ili usipoteze soga zako za video kwenye kichupo cha kivinjari au katika madirisha uliyofungua.
Simu za sauti na video kwenye WhatsApp hufumbwa mwisho hadi mwisho, kwa hivyo WhatsApp haiwezi kuzisikia au kuziona, iwe unapiga kutoka kwenye simu au kompyuta yako. Tunaanza kwa simu za mtu na mwenzake katika programu ya WhatsApp kwenye kompyuta ili kuhakikisha kwamba tunakupa huduma ya hali ya juu. Tutapanua kipengele hiki ili kujumuisha simu za sauti na za video kwa ajili ya vikundi katika siku zijazo.
Ni matarajio yetu kwamba watu watafurahia kuwapigia ndugu na marafiki zao simu kwa njia salama na ya faragha kwenye kompyuta. Unaweza kusoma zaidi, ikijumuisha jinsi ya kupakua programu ya eneo-kazi kwenye Windows PC na Mac hapa.