Tarehe 8 Desemba, 2020
WhatsApp inazidi kuwa jukwaa ambapo watu hujadili kuhusu bidhaa na kuratibu mauzo. Katalogi zimewasaidia watu kuona kwa haraka bidhaa zinazopatikana na kuzisaidia biashara kupanga soga zao ili kuambatana na bidhaa mahususi. Huku idadi ya ununuzi unaofanyika kupitia soga ikiendelea kuongezeka, tunataka kufanya mchakato wa ununuzi na uuzaji kuwa rahisi zaidi.
Kuanzia leo, ni fahari yetu kukuletea vikapu kwenye WhatsApp. Vikapu ni kipengele kizuri unapotuma ujumbe kwa biashara ambayo inauza bidhaa nyingi kwa mkupuo, kwa mfano, mkahawa au duka la nguo. Kwa kutumia vikapu, watu wanaweza kuvinjari katalogi, kuchagua bidhaa kadhaa na kutuma oda ikiwa ujumbe mmoja kwenda kwa biashara. Hatua hii itazirahisishia biashara kufuatilia maswali ya oda, kudhibiti maombi ya wateja na kufanya mauzo.
Kwa mfano, Agradaya, biashara endelevu ya mimea na manukato huko Yogyakarta, Indonesia ilipata ufikiaji wa mapema wa huduma hiyo na kutuambia jinsi vikapu ni njia rahisi ya kuelewa kile mteja anachoagiza bila mawasiliano ya mara kadhaa.
Ni rahisi kutumia vikapu. Tafuta tu bidhaa unazotaka kisha uguse “weka kwenye kikapu”. Ukishaweka vitu unavyohitaji kwenye kikapu, kitume kama ujumbe kwenda kwa biashara. Maelezo zaidi juu ya kutumia vikapu yanaweza kupatikana hapa.
Kipengele cha vikapu kitaanza kutumika kote duniani kuanzia leo -- wakati mwafaka kwa ajili ya msimu wa sikukuu. Furahia ununuzi kwenye WhatsApp!