Tarehe 6 Desemba, 2021
Lengo letu ni kufanikisha mawasiliano duniani kwa faragha. Huku mawasiliano yetu mengi yakizidi kuhamia mifumo ya dijitali kutoka ana kwa ana, tunatambua kwamba kuna upekee fulani wa kuketi na mtu na kushauriana naye uso kwa macho, mkielezana mawazo yenu kwa ujasiri, mkifahamu kwamba mnawasiliana kwa faragha na kwa wakati halisi. Uhuru wa kusema ukweli na kufungua roho, huku mkijua kwamba mazungumzo yenu hayanakiliwi na kuhifadhiwa mahali fulani milele.
Basi unafaa kuwa na uhuru wa kuamua ujumbe wako utadumu kwa muda gani. Tumezoea kuacha nakala dijitali ya karibu kila kitu tunachoandika hata bila kufikiria. Imekuwa kama daftari linaloandamana nasi kila mahali na kuunda rekodi ya kudumu ya kila kitu tunachosema. Hii ndiyo maana mwaka uliopita tulizindua ujumbe unaotoweka na hivi karibuni, tumeanzisha kipengele cha picha na video zinazotoweka pindi tu baada ya kuzitazama mara moja.
Leo tunafuraha ya kuwawezesha watumiaji wetu kuwa na udhibiti zaidi juu ya ujumbe wao na muda ambao ujumbe unadumu. Tuna vipengele vya kuwezesha ujumbe kutoweka kwa chaguomsingi, hali kadhalika vipindi tofauti vya muda ambao ujumbe unaweza kudumu.
Watumiaji wa WhatsApp sasa watakuwa na chaguo la kuwasha ujumbe unaotoweka kwenye soga zao zote mpya. Hali hii ikiwashwa, ujumbe wote mpya unaoanzisha ili kuwasiliana na mtu mwingine au ambao mtu anaanzisha ili kuwasiliana na wewe utatoweka baada ya muda uliochagua. Pia tumeongeza chaguo jipya wakati unaanzisha soga ya kikundi linalokuwezesha kuwasha hali hii unapoanzisha kikundi kipya. Kipengele hiki kipya ni cha hiari na hakibadili wala kufuta soga zako zozote zilizopo.
Pia tunaongeza chaguo mbili za muda ambao ujumbe unaotoweka utadumu: Saa 24 na siku 90, pamoja na chaguo lililopo la siku 7.
Kwa watu wanaochagua kuwasha hali ya ujumbe kutoweka kwa chaguomsingi, tunaonyesha ujumbe kwenye soga zako ili kuwajulisha watu muda chaguomsingi uliouchagua. Ujumbe huo hubainisha wazi kwamba si uamuzi unaomlenga mtu mmoja, bali ni chaguo la jinsi unavyotaka kuwasiliana na kila mtu kwenye WhatsApp kuanzia sasa kwenda mbele. Hata hivyo, kama ungependa ujumbe fulani udumu, ni rahisi kubadilisha.
Kutokuwa karibu na ndugu na marafiki kwa zaidi ya mwaka mmoja kumetudhihirishia wazi kwamba ingawa hatuwezi kuzungumza ana kwa ana, haimaanishi kwamba tunafaa kutojali faragha ya mawasiliano yetu ya binafsi. Tunaamini kuwa ujumbe unaotoweka pamoja na ufumbaji wa mwisho hadi mwisho ni vipengele viwili muhimu vinavyohimili jinsi ya kuwasiliana kwa faragha katika zama hizi. Vipengele hivi vinatuleta karibu na kupata hali sawa na mazungumzo ya ana kwa ana.
Ili uanze, nenda katika mipangilio ya Faragha kisha uchague ‘Muda Chaguomsingi wa Ujumbe’. Unaweza kupata maelezo zaidi hapa.