Tarehe 3 Agosti 2021
Ingawa kupiga picha na kurekodi video kwa simu zetu kumekuwa sehemu kubwa ya maisha yetu, si kila kitu tunachoshiriki kinafaa kuwa kumbukumbu ya kudumu ya kidijitali. Katika simu nyingi, ukipiga picha itachukua nafasi na kukaa katika hifadhi ya kamera yako daima.
Hii ndiyo sababu leo tunazindua picha na video za Kutazama Mara Moja ambazo zitatoweka kwenye soga baada ya kufunguliwa, hivyo kuwapa watumiaji uwezo zaidi wa kudhibiti faragha yao.
Kwa mfano, unaweza kutuma picha ya Kutazama Mara Moja ya nguo mpya unazojipima dukani, kutoa maoni ya haraka kuhusu jambo fulani, au taarifa fulani nyeti kama vile nenosiri la Wi-Fi.
Sawa na ujumbe mwingine wa binafsi unaotuma kwenye WhatsApp, maudhui ya Kutazama Mara Moja hufumbwa mwisho hadi mwisho kwa hivyo WhatsApp haiwezi kuyaona. Pia yatawekewa alama bayana ya aikoni ya “mara moja”.
Baada ya maudhui kutazamwa, ujumbe utaonekana ukiwa na neno “imefunguliwa” ili kuepusha mkanganyiko kuhusu kilichokuwa kikifanyika kwenye soga wakati wa maudhui hayo kutoweka.
Tunazindua kipengele hiki kwa kila mtu kuanzia wiki hii na tunatazamia kupata maoni kuhusu njia hii mpya ya kutuma maudhui ya faragha na yanayotoweka.
Unaweza kusoma zaidi kuhusu jinsi ya kukijaribu hapa.