Tarehe 18 Februari, 2021
Leo tunashiriki mipango iliyosasishwa kuhusu jinsi tutakavyowaomba watumiaji wa WhatsApp kuhakiki masharti yetu ya huduma na sera ya faragha. Hapo awali tulikabiliana na kiasi kikubwa cha taarifa zisizofaa kuhusu sasisho hili na tunazidi kujitahidi ili kuondoa mkanganyiko wowote.
Kumbuka, tunatengeneza njia mpya za kuwasiliana au kununua katika biashara zilizo kwenye WhatsApp, ni hiari kabisa kutumia njia hizo. Ujumbe wa binafsi utaendelea kufumbwa mwisho hadi mwisho kila wakati, kumaanisha kwamba WhatsApp haiwezi kusikia au kuusoma.
Tumetafakari kuhusu kile tungefanya kwa njia tofauti. Tungependa kila mtu ajue historia yetu ya kutetea ufumbaji wa mwisho hadi mwisho na aamini kwamba tumejitolea kulinda faragha na usalama wa watu. Sasa tunatumia sehemu ya Hali kushiriki maadili na masasisho yetu moja kwa moja kwenye WhatsApp. Tutafanya zaidi ili kuhakikisha kwamba tunaeleweka vizuri siku za usoni.
Katika wiki chache zijazo, tutaonyesha bango kwenye WhatsApp likiwa na maelezo zaidi ambayo watu wanaweza kuyasoma kwa wakati wao wenyewe. Pia tumejumuisha maelezo zaidi ili kujaribu kushughulikia baadhi ya madukuduku ambayo tunayasikia. Hatimaye, tutaanza kuwakumbusha watu wakague na kukubali masasisho haya ili waweze kuendelea kutumia WhatsApp.
Pia tunadhani ni muhimu kwa watu kujua jinsi tunavyoweza kutoa huduma za WhatsApp bila malipo. Kila siku, mamilioni ya watu huanzisha soga ya WhatsApp ili kuwasiliana na biashara kwa sababu ni rahisi zaidi ya kupiga simu au kuandikiana barua pepe. Tunatoza biashara ili ziweze kutoa huduma kwa wateja kwenye WhatsApp - hatutozi watu. Baadhi ya vipengele vya ununuzi huhusisha Facebook ili biashara ziweze kudhibiti orodha zao za bidhaa kwenye programu hizi. Tunaonyesha maelezo zaidi moja kwa moja kwenye WhatsApp ili watu waweze kuchagua ikiwa wanataka kuingiliana na biashara, au la.
Katika kipindi hiki, tunaelewa kwamba baadhi ya watu wanaweza kuangalia programu nyingine zilivyo. Tumeshuhudia baadhi ya washindani wetu wakijaribu kudai kwamba hawawezi kuona mawasiliano ya watu - ikiwa programu haina ufumbaji wa mwisho hadi mwisho kwa chaguomsingi, basi inaweza kusoma ujumbe wako. Baadhi ya programu zinadai kwamba ni bora kwa sababu zina taarifa chache ikilinganishwa na WhatsApp. Tunaamini kwamba watu wanataka programu ziwe salama na za uhakika, hata kama hilo linamaana kwamba WhatsApp itahitaji kiasi fulani cha data. Tunajitahidi kuwa waangalifu katika uamuzi tunaofanya na tutaendelea kubuni njia mpya za kutimiza majukumu haya kwa kutumia taarifa chache, si nyingi.
Tunamshukuru kwa dhati kila mtu ambaye ametusaidia kushughulikia changamoto hizi na bado tupo tayari kujibu maswali yoyote. Hatujaacha kubuni kwa ajili ya 2021 na tunatarajia tutakuwa na mengi ya kushiriki katika wiki na miezi ijayo.