Aprili 14, 2022
Leo tuna furaha kushiriki maono yetu kuhusu kipengele kipya tunachoongeza kwenye WhatsApp kinachojulikana kama Jumuiya. Tangu tulipozindua WhatsApp mwaka wa 2009, lengo letu limekuwa kuwasaidia watu kuwasiliana kwa njia inayokaribiana na mazungumzo ya ana kwa ana wanapotaka kuzungumza na mtu binafsi, kikundi cha marafiki au familia. Pia, mara kwa mara tunapokea maoni kutoka kwa watu wanaotumia WhatsApp kuwasiliana na kuratibu shughuli katika jumuiya.
Mashirika kama vile shule, vikundi vya kieneo na mashirika yasiyo ya faida sasa yanatumia WhatsApp kuwasiliana kwa njia salama na kutekeleza mambo — hasa baada ya janga kutuchochea kutafuta njia za ubunifu za kufanya kazi pamoja tukiwa sehemu mbalimbali. Kutokana na maoni mengi ambayo tumepokea, tunaamini kuwa kuna mengi tunayoweza kufanya ili kuwawezesha watu kudhibiti mazungumzo haya yanayofanyika sana katika vikundi hivi.
Yote haya yatawezekana kupitia kipengele cha Jumuiya. Jumuiya kwenye WhatsApp zitawawezesha watu kuleta pamoja vikundi tofauti katika jumuiya moja inayowafaa. Kupitia hili, watu wanaweza kupokea taarifa zinazotumwa kwenye Jumuiya nzima na kupanga kwa urahisi vikundi vidogo vya kujadiliana kuhusu yaliyo muhimu kwao. Jumuiya pia zitajumuisha zana mpya mahiri kwa wasimamizi, ikiwemo kudhibiti vikundi vinavyoweza kujumuishwa, na ujumbe wa kutaarifu unaotumwa kwa watu wote.
Tunaamini kuwa Jumuiya zitamwezesha mwalimu mkuu wa shule kuwaleta pamoja wazazi wote wa shule ili kushiriki nao habari muhimu na kuanzisha vikundi vya madarasa mbalimbali, shughuli za ziada, au uhisani.
Pia tunafanya maboresho kadhaa kuhusu jinsi vikundi hufanya kazi kwenye WhatsApp — iwe vikundi hivyo ni sehemu ya Jumuiya au la. Tunaamini maboresho haya yatasaidia watu kushiriki maudhui kwa njia mpya na yatapunguza upakiaji wa soga nyingi mno katika vikundi vyenye washiriki wengi. Vipengele hivi vitapatikana katika wiki zijazo ili watu waanze kuvijaribu hata kabla ya Jumuiya kuwa tayari.
Mawasiliano kwenye jumuiya ni ya faragha, ndio maana tutaendelea kulinda ujumbe kupitia ufumbaji wa mwisho hadi mwisho. Teknolojia hii ya usalama ni muhimu sana katika kulinda faragha na usalama wa watu. Vikundi vya watu wanaoshirikiana kwa ukaribu — shule, washirika wa kanisa, hata wafanyabiashara — wangependa na wanahitaji kuwa na mazungumzo salama na ya faragha bila WhatsApp kufuatilia kila wanachokifanya. Unaweza kupata maelezo zaidi kuhusu jinsi tunavyoshughulikia faragha, usalama na ulinzi wa jumuiya hapa.
Ingawa programu zingine zinabuni njia za kupiga soga kwa ajili ya mamia ya maelfu ya watu, tunalenga kusaidia vikundi ambavyo ni sehemu ya maisha yetu ya kila siku. Jumuiya kwenye WhatsApp ni huduma mpya hivyo lengo letu katika kipindi cha mwaka moja ujao ni kubuni vipengele vipya vitakavyotumika. Tunafuraha kuwaletea watumiaji huduma ya Jumuiya na tunatazamia kupokea maoni yao.