Tarehe 19 Julai, 2021
Katika kipindi ambapo wengi wetu tuko mbalimbali, hakuna kitu kizuri zaidi ya kujumuika na ndugu na marafiki katika simu ya kikundi. Pia hakuna kitu kibaya kama kutambua kwamba umekosa fursa hiyo adimu.
Jinsi umaarufu wa simu za vikundi unavyoendelea kukua, tumekuwa tukiboresha hali ya utumiaji kwa watumiaji wetu, huku pia tukiendelea kutoa usalama na faragha kupitia ufumbaji wa mwisho hadi mwisho.
Leo, tunaongeza uwezo wa kujiunga na simu ya kikundi, hata baada ya simu hiyo kuanza. Uwezo wa kujiunga na simu ikiwa tayari imeanza unaondoa ulazima wa kujibu simu ya kikundi pindi inapoanza. Hali hii inaleta haraka na urahisi kama wa mazungumzo ya ana kwa ana katika simu za vikundi kwenye WhatsApp.
Wakati mwingine mazungumzo mazuri zaidi hufanyika usipoyatarajia. Sasa, ikiwa mtu katika kikundi chako amekosa kupokea simu ilipopigwa, bado anaweza kujiunga wakati wowote anapopenda. Pia unaweza kuondoka kwenye simu na kujiunga tena wakati wowote mradi simu bado inaendelea.
Pia tumebuni skrini ya maelezo ya simu ili uweze kuona ni nani tayari amejiunga na nani amealikwa lakini bado hajajiunga. Kadhalika, ukigusa ‘puuza’ unaweza kujiunga baadaye kutoka kwenye kichupo cha simu kwenye WhatsApp.
Kipengele cha simu unazoweza kujiunga nazo kinazinduliwa leo na tunataraji kwamba watu wataanza kufurahia hali hii mpya.
Unaweza kusoma zaidi kuhusu jinsi ya kuijaribu hapa.