19 Mei, 2022
Kwa watu na biashara kote ulimwenguni, shughuli za kibiashara sasa zinafanyika kwenye WhatsApp. Iwe ni duka la rejareja au kampuni lililoorodheshwa kwenye jarida la Fortune 500, biashara kubwa na ndogo leo zinategemea WhatsApp katika kuwahudumia wateja wao.
Kama ambavyo WhatsApp imewezesha wapendwa kuwasiliana kwa urahisi wakiwa mbali, tungependa kushughulikia changamoto ambazo sote tumepitia tunapohitaji kuwasiliana na wafanyabiashara. Hii inamaanisha hakuna tena kusubiri muda mrefu, kukumbwa na hitilafu kwenye tovuti isiyofanya kazi, au kutuma barua pepe bila uhakika kuwa itasomwa.
Kufikia sasa, tumesaidia kuboresha mamilioni ya biashara kwa kutumia WhatsApp. Hatua inayofuata ni kutoa huduma ya WhatsApp kwa kila biashara inayohitaji kuwasiliana na wateja wake kwa njia rahisi, ya haraka na ya kutegemewa.
Leo tunachukua hatua muhimu katika kutoa huduma ya WhatsApp kwa biashara kubwa na ndogo kote ulimwenguni kupitia huduma salama zisizolipishwa za kupangisha programu kwenye wingu zinazotolewa na Meta. Kwa kutumia API hii mpya, tumepunguza muda wa kusubiri usajili kutoka miezi kadhaa hadi dakika chache ili biashara na wasanidi waweze kufikia huduma yetu haraka na kwa urahisi, kutumia mfumo wa WhatsApp ambao tayari upo ili kubadilisha hali ya utumiaji kuwafaa na kuweza kuwasiliana na wateja wao kwa haraka zaidi. Huduma hizi pia zitaondolea washirika wetu gharama kubwa za seva na zitawawezesha kufikia vipengele vipya papo hapo. Biashara zinaweza kujisajili moja kwa moja au kushirikiana na mmoja wa watoa huduma zetu za biashara ili kuanza.
Kwa miaka kadhaa sasa tumeona jinsi biashara ndogo ndogo zinazotumia WhatsApp zimekua, hivyo tungependa kutoa zana za ziada ili biashara hizi ziendelee kunawiri. Tunatarajia kuwa baadhi ya biashara zitapendelea kutumia API ya Wingu japo biashara nyingi zitaendelea kutumia programu ya WhatsApp Business. Pia tunasanidi vipengele vya kina vitakavyotumiwa na biashara hizi ili kuzisaidia kufikia wateja wengi na kujitangaza mtandaoni – kama vile uwezo wa kudhibiti soga kwenye hadi vifaa 10 ili kuziwezesha kushughulikia vyema soga nyingi. Pia tutatoa viungo vipya unavyoweza kubadilisha na vinavyokuwezesha kupiga soga kwenye WhatsApp unapobofya, ili kusaidia biashara kuvutia wateja kote mtandaoni. Tunapanga vyote hivi viwe vipengele vya ziada, vya kuchagua na vinavyolipishwa kwenye programu ya WhatsApp Business kama sehemu ya huduma mpya inayolipishwa. Tutashiriki maelezo zaidi baadaye.
Njia hizi mpya za kusaidia biashara haziathiri maadili yetu kuhusiana na mazungumzo kati ya mtu na biashara. Wewe ndiye unadhibiti soga kati yako na biashara na hutapokea ujumbe kutoka kwa biashara ikiwa hujawaomba wawasiliane nawe.
Tunatumai watu watafurahia kupiga soga na biashara wanazozipenda kwenye WhatsApp, na ni matarajio yetu kuwa biashara mpya zitachipuka, zitajikuza na zitastawi.